Taasisi ya Umoja wa Afrika inayohusika na ukuzaji wa lugha (ACALAN) inaendelea kuhamasisha Waafrika kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano mapana.

Kiswahili kimerasmishwa na Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADEC) kutokana na umuhimu wake.

Shirila la Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kwa upande wake limetenga siku maalum kwa ajili ya Kiswahili, ambayo ni kila tarehe 7 Julai.

Lakini baadhi ya Waafrika wanaohamasishwa kukipenda Kiswahili wana lugha zao zingine, hata hawajui kuna lugha inaitwa Kiswahili.

Je, ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili utakuwa rahisi? Nimezungumza na Prof. Aldin Mutembei, Mwenyekiti wa Kigoda cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akiwa safarini nchini Rwanda, nimemuuliza kwanza kwa nini Kiswahili ndicho kinapigiwa upatu ilhali Afrika ina lugha chungu nzima.

Prof Mutembei: Kwanza Kiswahili ni lugha ya pekee kwa kuwa haijikiti kwenye kabila fulani, haijikiti kwenye jamii moja, kwa maana kamba ukiiendelea lugha hiyo unawaendeleza watu wa kabila hilo au wa jamii hiyo.

Ni sawa sawa na kwamba Tanzania pia tuna lugha nyingi sana lakini ilichaguliwa Kiswahili kwa sababu ni lugha ambayo kuwapo kwake kumetoka Kusini mwa Somalia na kuenea ukanda wote wa Afrika Mashariki mpaka Kaskazini mwa Msumbiji na mpaka leo huwezi kusema kwamba hawa ni Waswahili kama kabila.

Kwa hiyo hata ilipochaguliwa Tanzania ilichaguliwa kwa sababu haikuwa inaendeleza ukabila wa lugha fulani. Hili ni jambo moja ambalo linakipa Kiswahili nafasi ya pekee.

Sababu ya pili, katika lugha za Afrika lugha pekee ambayo imefundishwa kuliko lugha zote na hata nje kule ni lugha ya Kiswahili.

Huko nje iwe ni Ulaya, Amerika, Canada, Kusini mwa Amerika, wanafunzi wanapojifunza lugha za Kiafrika lugha ambayo wanaichagua kwa wingi wake ni lugha ya Kiswahili.

Janvier Popote: Kwa nini?

Prof Mutembei: Ni kwa sababu mawazo ya watu kule nje wanafikiri Afrika ni nchi moja kama ambavyo ungekuwa unakwenda India, Rwanda. Wanapofikiria Afrika wanafikiri ni nchi moja.

Nakumbuka pia hotuba ya Mwalimu Nyerere kabla hajafa alikwenda kule katika bunge la Afrika Kusini na kuhutubia bunge na kuwaambia, “Mnajua japo huko nje wanaona Afrika kama kitu kimoja hivi na mimi nadhani ni sawa, sisi wote tuwe wamoja sasa tuende kwa pamoja.”

Sasa wanafunzi wanapokuwa kule nje wanafikiri Afrika ni moja mpaka wafundishwe kuhusu jeografia ya Afrika na nchi zilizopo Afrika na kadhalika.

Wanadhani wakijifunza Kiswahili ni lugha ambayo itaweza kuwapeleka nchi zote za Afrika kwa sababu wanadhani Waafrika wote wanazungumza Kiswahili.

Lakini jambo jingine ni kwamba, tokea zamani lugha hii ya Kiswahili ilikuwa ni sawa kama ni lugha ya Kiarabu, ina asili ya Uarabu lakini hii ni lugha ya kibantu.

Kwa hivyo Wabantu wengi ambao ndio wengi Afrika wakizungumza tunasikilizana. Mfano Mnyarwanda akizungunza na mtu kutoka Burundi akizungumza na Wahangaza wana lugha inaitwa Lufumbila lugha zao zinaelekeana kwa sababu wote ni Wabantu.

Mbantu wa Afrika Kusini na Mbantu wa Afrika Magharibu, Kameruni, maneno kadhaa yanaelekeana. Kwa hivyo Kiswahili, kwa sababu ni lugha ya kibantu, ni rahisi kujifunza, kina msamiati unaofanana, kina muundo wa lugha unaofanana na kadhalika. Kwa hivyo ni rahisi kwa Waafrika wengi kujifunza lugha ya Kiswahili.

Na jambo la mwisho, wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili duniani ni kama watu miliyoni mia mbili hamsini hivi, na ni lugha ambayo miaka ya sitini walipendekeza kwamba ndiyo ilitakiwa kuwa lugha inayotuunganisha sote kama Waafrika.

Hata Wole Soyinka kutoka Nigeria hazungumzi Kiswahili lakini alisema hii ndiyo lugha iliyotakiwa kuwa lugha ya fasihi ya Afrika kwa sababu anaona hii ndiyo lugha ambayo ikiendelezwa inaweza ikawapeleka Waafrika wakawa na sauti moja kama alivyokuwa amesema Kwame Nkrumah.

Yeye mwenyewe hazungumzi Kiswahili lakini alisema, mwaka 1962, akimuambia Mwalimu Nyerere kwamba anapendekeza ikiwa Waafrika watakuwa na sauti moja basi sauti hiyo iwe ni lugha ya Kiswahili.

Kwa hivyo Kiswahili kikawa na muelekeo, kikawa kimeandikwa sana, kimeandikwa na watu wa nje, kimeandikwa na watu wa ndani, kimefanyiwa utafiti mwingi sana, kinafundishwa kiurahisi, watu wamejifunza kiurahisi, kwa hivyo kimejikuta kiko katika hadhi hiyo, na leo tunapozungumza juu ya Kiswahili si cha Tanzania, si cha Kenya, si cha Rwanda, wala Burundi wala Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ni cha Waafrika.

Wale ambao walikuwa Tanzania wakati wa kupambana kukomboa nchi zao wanajua kwamba lugha ya Kiswahili iliwaunganisha kama lugha ya ukombozi. Walikuwa jeshini wakijifunza lugha ya Kiswahili wakiwasiliana kwa lugha ya Kiswahili dhidi ya maadui wao.

Kwa hiyo Kiswahili kimeenea katika nchi za Namibia, Zimbabwe, Afrika Kusini, hata Zambia, Malawi, Msumbiji, Guinea Bissau, kote huko ambako watu walikuwa wamekaa katika Afrika Mashariki kwa ajili ya kupigania nchi zao au kuondoa ubaguzi wa rangi walijifunza Kiswahili. Kwa hivyo imekuwa ni lugha kwao kama lugha ya ukombozi.

Janvier Popote: Kuna rafiki yangu mmoja wa Mauritania na mwingine wa Senegal wote waliniambia hawajui lugha inaitwa Kiswahili. Watakipendaje Kiswahili, watakithaminije na kukipa kipaumbele maishani mwao? Unadhani safari ya kuwahamasisha ni rahisi?

Prof Mutembei: Kwamba ni rahisi au si rahisi si neno sana. Lakini kwamba tumeanza hili ni la muhimu. Kwa sababu ukiogopa kuvuka mto hata kabla hujakaribia utapata tatizo, unafika kwenye mto unakumbana na matatizo yaliyopo ndipo unasema sasa katika mto huu na ukubwa huu nitaweza kuruka, hapana sitaruka nitaweza kuogelea au hapana nitaweka miti kama daraja na kadhalika.

Kwa hivyo tunajua kabisa wala si leo na si jana, zamani, tunajuwa kwamba wapo watu ambao hawana habari juu ya lugha ya Kiswahili. Kama ambavyo kuna wengine ambao hawana habari kuhusu nchi. Kama nilivyokuambia mwanzoni, wanadhani Afrika ni nchi moja.

Nakumbuka wakati wa kugombea urais kule Marekani, Rais Bush alikuwa hajui sana mambo ya Afrika, walimuambia kuhusu Tanzania akasema Tasmania, walimuambia kuhusu Nigeria walikuwa wanamuuliza maswali akadhani kwamba labda ni sehemu fulani iko Alaska au hivi, alijua Afrika ni nchi, kwa hivyo sitashangaa kwamba watu hawajui hata kuhusu lugha ya Kiswahili.

Kitu muhimu ni kwamba tumeanza safari au tunaendeleza kwa kweli safari yenyewe na tutatumia mbinu mbalimbali ili kuwafanya hao ambao hawajui kwamba Afrika ni bara na lina nchi mbalimbali, hawajui kwamba lugha ya Kiswahili ni lugha kama lugha nyingine, kwa mfano kwa taarifa yako bara la Afrika kuliko bara la Ulaya likiunganishwa na Uchina likiunganishwa na bara lote la Amerika ukiweka kwa pamoja. Kwa hivyo kwa maana ya kilomita za mraba Afrika ni kubwa sana. Lakini ukiangalia ramani tuliyo nayo imechorwa kuonesha kwamba Afrika ni ndogo. Ni hivyo hivyo.

Nimefikia huo mfano kusudi uweze kuelewa kwamba watu wanadhani Kiswahili ni kalugha kadogo lakini ni lugha ya watu miliyoni mbia mbili hamsini.

Prof Mutembei akiwa katika mkutano wa ACALAN kuhusu uendelezaji wa Kiswahili barani Afrika (Picha/Janvier Popote)

LEAVE A REPLY