Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia suluhu Hassan amesema uhusiano uliopo kati ya nchi hiyo na Kenya hauwezi kuvunjika akibainisha kuwa  wapo watu wenye nia ovu wanaotamani kuona umevunjika.

Ametoa kauli hiyo Jumatano Mei 5, 2021 wakati akilihutubia Bunge la Kenya mara baada ya kumalizika kwa kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya.

“Binafsi huwa nashangazwa sana na wale wanaodhani Kenya na Tanzania ni wapinzani, mbaya zaidi ni kule kuamini kwao kwamba hilo linawezekana tu mmoja wetu kumwangusha mwenzake,  hawa ni watu wenye mioyo ya choyo, maono mafupi na akili mbovu.”

“Ni bahati mbaya kuwa watu hawa wapo katika pande zote mbili, Kenya na Tanzania hutokea pia wachache wao wakawa ni watumishi wa Serikali zetu na hata wanasiasa wa pande mbili za nchi zetu. Bahati nzuri ni kuwa si wengi ndio maana uhusiano wa nchi zetu mbili unatimiza miaka 56 sasa,” amesema Samia.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ameahidi katika uongozi wake atahakikisha kuwa Kenya inabaki kuwa ndugu, jirani, mshirika wa mkakati na mbia kwa kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili umefungwa katika mafundo matatu.

Ameyataja mafundo hayo kuwa ni undugu wa damu ambao hauwezi kutenganishwa na mipaka ya kuchorwa kwenye ramani, fundo la kihistoria na la kijiografia.

“Ushirikiano wetu si wa hiari bali wa lazima kutokana na kanuni ya uasili wa undugu ambao Mwenyezi Mungu ameuumba, ushirika na ujirani yote yanatufanya tuwe pamoja hili la maumbile hatuna uwezo wa kulibadilisha kilichobaki ama tupendane au tuchukiane hatuwezi kukwepa kutokana na mafundo haya matatu yaliyowekwa pamoja, tunategemeana kwa kila hali iwe kheri au shari.”

“Panapotokea ukame Tanzania njaa inabisha hodi Kenya, uzalishaji wa viwanda ukisimama Kenya bidhaa zinakosekana Tanzania hivyo hatuna budi kupatana na kuishi kwa neema na furaha,” amesema Samia.

Chanzo: Mwananchi

LEAVE A REPLY