Msanii wa Afrobeat Mico da Best

Msanii wa Rwanda wa ngoma za miondoko ya Afrobeat, Mico da Best, amesema kama kuna kipindi kigumu ambacho wasanii wa Rwanda waliwahi kupitia ni hiki cha janga la Korona.

Kuanzia mwezi wa tatu, wasanii hawaruhusiwi kufanya matamasha kutokana na shughuli hizo kupigwa marufuku kama sehemu ya mikusanyiko inayoweza kuwa chachu ya kusambaa kwa COVID-19.

“Shughuli nyingi ambazo zinaweza kumpa kipato msanii hazipo, watu wanauliza wasanii mnaishije, wengine wanapendekeza serikali itoe misaada maalum kwa wasanii,” amesema Mico.

Mico amesema wakati serikali inatoa misaada ya vyakula kwa kaya zisizojiweza wiki chache baada ya kutangazwa marufuku ya kutotoka nje, wasanii waliofulia walishindwa kujitokeza kuomba misaada.

“Wasanii ni watu ambao wanajisikia sana hawezi kuenda sehemu ambazo chakula kinatolewa, naweza kusema kwamba hii hali ni hatari kwa wasanii,” ameongeza Mico.

Kutokana na umaarufu wao, wasanii wamekuwa wakilipuuzia mbali suala la wao kujitokeza kwa ajili ya kupewa chakula kilichogawiwa na serikali, wakiona itawashushia hadhi.

Serikali ilipotangaza marufuku ya kutotoka nje ili kudhibiti kuenea kwa Virusi vya Korona, wachungaji wa makanisa walitoa mwito kwa waumini wao kufuatilia mahubiri kupitia mtandao wa Youtube.

Wakritso walitakiwa kutoa sadaka kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ya Mobile Money na Benki pia, njia ambayo hata wasanii walianza kuitumia japo haikuzaa matunda kama walivyotegemea.

Shoo ya Tuff Gang ilienda mrama baada ya wasanii hao kutoweka mita moja kati ya mtu na mtu mwingine, hali iliyokuja kutafsiriwa kama ukiukwaji wa tahadhari za kupambana na Virusi vya Korona.

Shoo hiyo ya ‘live’ ya Mei 24, ilizuiliwa na Jeshi la Polisi muda mfupi tangu ianze na kuwaingiza hasara waandaji wake.

“Ukiangalia hizi concerts ambazo watu wanapiga online siwezi nikakuambia kwamba zinatoa kitu”, amesema Bwana Mico katika mahojiano na Popote.rw

“Mimi ni msanii ambaye hufuata maelekezo ya serikali, siwezi nikaenda pembeni ama nilete mambo yangu, lakini nilihuzunika watoto wanatafuta chakula halafu wanawazuia.

Nimekuja kugundua kwamba kuna makosa wamefanya, unajua serikali iko pale kuangalia vitu ambavyo watu wa nje hawaoni.”

Mico da Best amewashauri wasanii wenzake kujihakikishia vitega uchumi vingine ili kwamba kama muziki ukiwa na matatizo basi wawe na sehemu nyingine ya kukimbilia.

Amesema kuna msanii mwenzake ambaye alimuambia kwamba anaona biashara ya kuuza duka ni bora kuliko muziki maana maduka yaliendelea kufanya kazi wakati muziki umepigwa marufuku.

“Hali kama hii ya Covid imefanya wasanii waonekane kwa picha nyingine,” ameongeza Bwana Mico.

Bofya hapa kuangaliwa wimbo anaotamba nao wa Igare

Mwandishi: Janvier Popote

LEAVE A REPLY