Jeshi la Polisi la Rwanda (RNP) likishirikiana na Idara ya Upelelezi (RIB) wamemtia nguvuni Bi Idamange Iryamugwiza Yvonne.

Mwanamke huyu mkazi wa Kimironko mjini Kigali, amekuwa akitoa matamshi makali dhidi ya Serikali ya Rwanda tangu Januari 31, 2021, kupitia chaneli yake ya Youtube.

Katika video yake ya kwanza, aliituhumu serikali kwa kuminya uhuru wa wananchi kwa kisingizio cha gonjwa mtandavu la Covid-19. Wakati huo wakazi wa Mji wa Kigali walikuwa wamewekewa marufuku ya kutoondoka nyumbani huku wakazi wa mikoani wakiwa hawaruhusiwi kuvuka mpaka  wa wilaya moja kuingia wilaya jirani.

Bi Idamange pia alisema serikali imekuwa ikitumia turufu ya mauaji ya kimbari yaliyotekelezwa mwaka 1994 dhidi ya Watutsi kuwakandamiza wapinzani.

Tume ya Taifa ya kupambana na itikadi za mauaji ya kimbari (CNLG) ilidai kuchukizwa na kauli za mwanamke huyu aliposema serikali huuza miili ya waliopoteza maisha katika mauaji ya kimbari kwa kuwaanika katika nyumba za makumbusho ya mauaji husika.

Katika video yake ya mwisho kupandishwa Youtube, jana Jumatatu Bi Idamange amesema serikali ilijaribu kumnunua kupitia Naibu Waziri katika Wizara ya Utamaduni, Edouard Bamporiki kwa lengo la kumnyamazisha lakini alikataa.

Katika video hiyo, ameinyooshea kidole serikali na kuihusisha na mauaji ya watu wengi wakiwemo tajiri Assinapol Rwigara aliyepoteza maisha katika ajali mwaka 2015, msanii Kizito Mihigo ambaye Polisi walisema alijiua mwenyewe akiwa katika Kituo cha Polisi cha Remera, mwanamitindo Alexia Mupende aliyeripotiwa kuuawa na mfanyakazi wake wa ndani, Luteni Jenerali Jacques Musemakweli aliyetangazwa kufariki dunia kwa ugonjwa wiki jana na wengineo wengi.

Wote hao, Idamange amesema wameuawa na serikali na kuongeza kwamba hata yeye yuko tayari kuuawa ama kutupwa jela lakini hana woga, akisema ameamua kuwatetea Wanyarwanda waliochoka kuongozwa kimabavu na haogopi chochote kwani ametumwa na Mungu.

Mwanamke huyu amefikia hatua ya kusema Rais Paul Kagame alifariki dunia muda mrefu uliopita lakini serikali haikutangaza kifo chake, na kuongeza kuwa Wanyarwanda ni kama kondoo wasiokuwa na mchungaji.

Bi Idamange amewataka Wanyarwanda kukutana Ikulu ifikapo saa tatu asubuhi (Jumanne, Februari 16, 2021) kwa ajili ya maandamano na kuomba Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi kuwahakikishia usalama.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, CP John Bosco Kabera amesema wakati wa kumkamata mwanamke huyu, alimjeruhi kichwani kwa kumpiga chupa afisa wa Polisi ambaye amewahishwa Hospitali ya Kacyiru kwa matibabu.

Bi Idamange, mama wa watoto wanne, anakabiliwa na madai lukuki ikiwemo kuhatarisha utulivu wa umma, kosa la jinai ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka hadi 15.

Imeandikwa na Janvier Popote

LEAVE A REPLY