Bi Judith Niyonizera ambaye alioana na msanii Safi Madiba kutokea nchini Rwanda, amekanusha taarifa za kutalikiana na mwanaume huyo ambaye walifunga ndoa ya kiserikali mnamo Oktoba 1, 2017.

“Sijaachana naye” amethibitisha Judith huku akipunga mkono kuwaonesha waandishi wa habari pete ya uchumba aliyovishwa na Safi. “Hizo taarifa hazina ukweli ndani yake” ameongeza.

Watu wameshangazwa na kitendo hicho cha yeye kutupilia mbali habari hizo ilhali zilitolewa na Safi mwenyewe miezi mitatu iliyopita, akisema yeye na Judith kila mmoja ameshachukua hamsini zake.

“Tulikosa maelewano. Watu wanaweza wasikubaliane tabia na vitu vingine. Nimetalikiana na mke wangu, sina la ziada. Wengine wanaweza wasiwe na uhakika lakini ndiyo hivyo.”

Nini chanzo cha mfarakano wao lakini? Kwa mujibu wa maelezo ya Safi, mwanamke huyu alimtesa kisaikolojia walikokuwa wanaishi pamoja nchini Canada, ambapo ilifika hatua ya Safi kumshtaki.

Taarifa zinasema Safi aliwafikishia malalamiko yake viongozi wa ngazi za chini za huko Canada baada ya pasi yake ya usafiri kushikiliwa na Judith, ambapo baadaye Safi aliihama kaya na kuenda kuishi na rafiki.

Safi alihamia Canada mapema mwaka huu, alipoondoka watu wakafikiri kwamba anakwenda kunogesha ndoa yake na Judith kumbe alipofika huko mambo yakaenda mbagombago kiasi cha kusababisha talaka.

Habari za chini ya kapeti zilisema Safi amerudiana na mpenzi wake wa zamani Umutesi Parfine, kitendo kilichomkasirisha mkewe Judith japo Judith amekanusha habari hizo akisema hazina unyayo wala utosi.

“Hiyo si kweli, sijamkasirikia, kwa kawaida sina ghadhabu”, alisema Judith jana Novemba 9, mjini Kigali akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa tahmthilia yake.

Alipoulizwa kama ana urafiki na Parfine, akasema urafiki haupo lakini hata uadui haupo maana hakujawa na sababu ya wao kuwa maadui.

Alipoulizwa maswali mengine kuhusu kuvunjika ndoa yake na Safi alionekana kuchukizwa na maswali hayo ya Bwana Chita. “Tumekuja kuzungumzia filamu siyo ndoa yangu. Naomba tuishie hapa.”

“Za nduru’

Kuhusu picha zilizoenea juzikati zikimuonesha Judith akivishwa pete ya uchumba huku ikisemekana amevishwa pete hiyo na mpenzi mpya, Judith amesema tafsiri hiyo ni potofu.

Amesema picha zilizoonekana zilichukuliwa kama sehemu ya utengenezaji wa tamthilia yake ya ‘Za nduru’ ambayo inazungumzia maisha na misoto ya wasanii ambayo mashabiki hawajui.

“Ni picha za tamthilia ambayo hata mimi ni muigizaji, mtaona hata picha zingine.”

‘Za nduru’ ni tamthilia ambayo wazo lake lilitoka kwa Alex Muyoboke ambaye amejizolea umaarufu kutokana na usimamizi wake wa kazi za wasanii kibao, huku udhamini wake ukitolewa na Judith.

Filamu itaanza kuoneshwa kupitia mtandao wa kijamii wa Youtube katika siku za hivi karibuni, lakini inaweza hata kuoneshwa kwenye vituo vya runinga, kwa mujibu wa Muyoboke.

Kuhusu maudhui ya filamu, Muyoboke amesema filamu itaangazia ‘maisha ya nyuma ya pazia’ ya wasanii ambayo wapenzi wa muziki hawayajui, ikiwa ni pamoja na mafanikio na misoto pia.

“Msanii anaweza kutoa wimbo wa pesa ndogo ila ukimuuliza kama video yake iligharimu kiasi gani akakuambia faranga miliyoni nane. Hayo yote nayajua subirini kuyaona kwenye filamu”, amesema.

Judith ambaye pia ni muigizaji, alijulikana hasa kupitia penzi lake na Safi. Hakuwa maarufu kabla ya hapo na jina lake ni geni katika ulingo wa filamu nchini Rwanda japo anasisitiza anajua kuigiza.

“Nilishawahi kuigiza filamu lukuki enzi za shule ya msingi na sekondari hadi nikapewa jina la ‘Masera’ (sista) na nimekuwa nalo hadi juzijuzi, mimi ni muigizaji stadi”, amesema Judith.

“Nilipofika Canada kuna wasanii wa Hollywood walinishirikisha kwenye filamu zao nikaigiza japo hazikutoka,” ameongeza Bi Judith akiwataka wapenzi wa filamu wakae mkao wa kula.

Imeandikwa na Janvier Popote

LEAVE A REPLY