Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Septemba 15, 2019. REUTERS/Amir Cohen/File Photo

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameikosoa idara ya haki nchini humo, kwa kumhusisha na makosa yasiyokuwa na msingi kwa lengo la kumng’oa madarakani ili kumpa nguvu mpinzani wake.

Netanyahu ambaye ni waziri mkuu wa kwanza wa Israel kuwahi kushtakiwa akiwa madarakani, yupo Mashariki mwa Jerusalem kuhudhuria vikao vya mahakama inayosikiliza kesi dhidi yake.

Netanyahu mwenye umri wa miaka 70, anatuhumiwa kwa makosa ya udanganyifu, kupoteza uaminifu na rushwa. Benjamin Netanyahu ambaye ameweka historia ya kuwa Waziri Mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini Israel, amesema kesi kesi yake inalenga kumwangusha ‘Waziri Mkuu mwenye nguvu’.

Hivi karibuni Wabunge waliidhinisha serikali ya muungano kati ya Benjamin Netanyahu na mpinzani wake mkuu Benny Gantz itakayoongozwa kwa miaka mitatu kwa kura 73 dhidi ya 46 za waliopinga na mbunge mmoja hakuhudhuria. Bunge la Israel lina viti 120.

Serikali hiyo mpya iliyopitishwa baada ya siku 500 za kutokuwepo na serikali thabiti imejiandaa kukabiliana na mizozo mikubwa katika wiki zake za mwanzo ikiwa ni pamoja na kuanguka kwa uchumi kulikosababishwa na janga la virusi vya Corona.

Waziri mkuu Benjamin Netenyahu anaongoza taifa hilo kwa miezi 18 kabla ya mpinzani wake mkuu Benny Gantz kuchukuwa hatamu za uongozi, kwa mjibu wa makubaliano yao.

Makubaliano hayo hata hivyo, yamesababisha kusambaratika kwa chama cha Gantz cha Bluu na Nyeupe, na kuvunja ahadi yake ya kampeni ya kutohudumu chini ya Netanyahu, anaesubiri kupandishwa kizimbani kwa mashtaka ya rushwa.

Chanzo: RFI

LEAVE A REPLY