Na Janvier Popote
Mnamo Novemba 19, 2020, chombo cha habari cha Uingereza (BBC) kilirusha ripoti yenye kichwa, “Le serment de loyauté qui terrorise les Rwandais de la diaspora”, maana yake ikiwa ni “Kiapo cha utiifu kinachowaogofya Wanyarwanda waishio ugenini.”
Mhimili wa ripoti hiyo ni picha zilizowaonesha Wanyarwanda wakiwa katika ukumbi wa Ubalozi wa Rwanda mjini London, wakiapa kuunga mkono chama tawala cha RPF-Inkotanyi.
Katika kiapo hicho, wanasema, “Nikisaliti ama kujitenga na mipango na matakwa ya RPF, nitakuwa nimewasaliti Wanyarwanda wote na itabidi niadhibiwe kwa kusulubiwa”.
Hiyo ndiyo kauli ya waliokula yamini kwa lugha ya Kinyarwanda, huku wakiahidi kusimama kidete dhidi ya “maadui wa Rwanda popote pale walipo.”
Kiapo hicho kimetafsiriwa kama ishara ya vitendo vya serikali ya Rwanda kuwafuata wapinzani wake kila wakimbiliako duniani kote, huku serikali hiyo ikilinganishwa na Korea Kaskazini.
Ubalozi wa Rwanda mjini London umesema hafla hiyo ilifanyika mnamo mwaka 2017, na kuhoji kwa nini BBC ikakubali kuchapisha habari yenye kupotosha hadhira yake.
“BBC imepitisha madai hayo kana kwamba ni ukweli, bila kuchunguza yakini yake au uaminifu wa waliotoa matamshi hayo,” Ubalozi umesema ukikosoa ripoti husika.
“Wanyarwanda wengi waishio ugenini walioamua kuwa wanachama wa RPF wamekuwa wakila kiapo cha utiifu kwa chama hicho kwa miaka 30, leo hakuna jipya kuhusu kiapo au kitendo cha Ubalozi kutoa nafasi kwa ajili ya tukio la umma.”
“Kiapo hicho kimekuwepo tangu kuundwa RPF mwaka 1987 na ni kama hakijabadilika. Wapinzani wanaojaribu kukifanya kionekane kama tishio wanatia huruma,” umeongeza Ubalozi.
Wapinzani wameiambia BBC kuwa matukio ya kiapo cha utiifu kwa chama tawala yamefanyika mara nyingi na lengo lake hasa ni kuwatia woga na kulazimisha uungaji mkono.
Mmoja wao amenukuliwa akisema watu wake wa karibu waishio nchini Rwanda wametekwa nyara na inawezekana wameuawa ili kumuadhibu yeye baada ya kugoma kula kiapo.
Hata hivyo, Ubalozi wa Rwanda mjini London umekosoa habari hiyo ya BBC, ukihoji kwa nini BBC ikaongea tu na wapinzani na wale wanaoomba hadhi ya ukimbizi kwa kulaghai.
“Mfano ni René Mugenzi ambaye majuzi alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo kwa ubadhirifu na wizi nchini Uingereza. Hata hivyo, Mugenzi amekuwa akipambwa kama mpigania haki na kiongozi wa upinzani na kupewa nafasi kubwa katika vyombo vya habari, hususan BBC ili kuisingizia Rwanda,” umesema Ubalozi.
Tukio la kuapa lilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ubalozi wa Rwanda nchini Uingereza, walioapa wakionekana kufikia 30 kulingana na video iliyosambaa katika mtandao wa Whatsapp.
BBC imesema, ingawa baadhi wanakipenda chama tawala kwa moyo mkunjufu, lakini wengine waliokula kiapo walifanya hivyo kwa kuhofia maisha yao kuingia mashakani.
Mmoja wao alinukuliwa akisema, “Nina uhakika idadi kubwa hawakuamini walichokiapa. Tulidanganya ili kujilinda na kuzilinda familia zetu ziishizo nchini Rwanda.”
Rwanda imetupilia mbali madai hayo ikisema wapinzani wake waishio ugenini huwa hawashiriki matukio yanayoandaliwa na Ubalozi.
“Wameona ni bora kutengeneza habari za kizushi kama hii ambazo hupokelewa kwa mikono miwili na BBC.”
Ubalozi umeongeza, “Wanyarwanda waishio Uingereza wanaounga mkono Serikali ya Rwanda ama RPF, hawakupewa nafasi ya kutoa maoni yao katika habari hii ya Harding.”
Mmoja ya wapinzani wa Serikali ya Rwanda aliyepewa nafasi ya kuzungumza katika ripoti hiyo ya BBC ni David Himbara ambaye aliwahi kuwa mshauri wa kiuchumi wa Rais Paul Kagame.
“Imezoeleka. Unaapa au unakuwa adui. Unachagua kunyoa ama kusuka”, amesema Himbara, ambaye ni mkazi wa Canada baada ya kufarakana na Rais Kagame.
Himbara ni mtu asiyeridhika, kwa mujibu wa Serikali ya Rwanda, ambaye amekuwa akiukosoa mfumo wa kisiasa wa Rwanda bila kukosolewa, ilhali maoni yake ni ya kupotosha.
“BBC wangetaka kuchunguza ukweli wa maoni yake, wangeiwezesha hadhira yao kuelewa kwamba, kwa jinsi chama tawala kilivyo pendwa, hakuna anayelazimishwa kujiunga nacho.”
Ubalozi umeongeza, “Hakika kuna vyama vingine 11 vya kisiasa, angalau vitano vimewakilishwa bungeni. Na kwa mujibu wa Katiba ya Rwanda, matawi mawili ya Bunge yanaongozwa na viongozi wa vyama vingine ambavyo hali ilivyo sasa vilikuwepo hata kabla ya RPF kuingia madarakani.”
BBC imesema imepata habari za kuaminika kwamba Serikali ya Rwanda imelenga kuwahujumu wapinzani wake walio ugenini huku pia ikiwalenga wanafamilia wao walioko nchini Rwanda.
“Ili kunitia woga, waliwapoteza ndugu zangu wawili. Kamwe hawakujihusisha na siasa. Walikuwa kwenye ardhi ya Rwanda. Kwa nini ikawa hivyo wakati hawajafanya chochote?”, alinukuliwa Noël Zihabamwe kutoka nyumbani kwake Australia.
BBC imesema mwanaume huyo anakaa Sydney baada ya kuwasili nchini Australia mwaka 2006 akikimbia vitisho vya serikali ya Rwanda aliyoyitaja kuwa inazidi kuwa ya kimabavu.
Hata hivyo, Ubalozi wa Rwanda nchini Uingereza umesisitiza kuwa Bwana Zibahamwe aliondoka nchini Rwanda mwaka 2010 na si 2016 kama BBC ilivyoripoti, “kwa lengo la kwenda kusoma kwa udhamini wa Serikali ya Rwanda.”
“Baada ya kuhitimu, Zibahamwe aliomba uraia wa Australia na baadaye kujiunga na kundi la kigaidi la Rwanda National Congress (RNC) ambalo hueneza uvumi dhidi ya serikali ya Rwanda,” Ubalozi umesema.
Rwanda imelitaja kundi la RNC kuwa lilihusika na mashambulizi mengi ya kigaidi yaliyotekelezwa mjini Kigali na Mkoa wa Kaskazini pia.
“Madai ya Zibahamwe kwamba ndugu zake wawili walipotezwa hayana ukweli. Mke wa miongoni mwa wanaume waliotajwa kuwa wametekwa nyara aliripoti Polisi na kusema mumewe hajulikani aliko tangu alipowatembelea wanafamilia wake wilayani Nyagatare.”
Ubalozi umeongeza, “Wakati upelelezi ukiendelea, iwe Zibahamwe ambaye anaendelea na uasi wake, iwe familia yake, hawatoi taarifa zaidi kusaidia kuthibitisha madai hayo.”
Taarifa ya Ubalozi wa Rwanda imetamatishwa kwa kusisitiza kwamba Rwanda imepania kuboresha maisha ya wananchi na haitawasikiliza watu wa nje wasioyaelewa maslahi ya raia wake.
“Ieleweke kwamba maadili ya msingi ya Rwanda na maamuzi ya kisiasa huongozwa na historia na muktadha wa nchi yetu na hulenga kuimarisha utulivu na ustawi, na pia mustakabali mzuri wa raia wetu. Hatutakubali hii kuvurugika,” imeishia hapa taarifa ya Ubalozi.