Rais wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa ametangaza kujiuzulu baada ya waandamanaji kuvamia makazi yake rasmi na kuchoma moto nyumba ya waziri mkuu.

Rais na waziri mkuu hawakuwa kwenye kwenye majengo wakati huo.

Mamia kwa maelfu waliwasili katika mji mkuu wa Colombo, wakimtaka Bw Rajapaksa ajiuzulu baada ya miezi kadhaa ya maandamano kuhusu usimamizi mbovu wa kiuchumi.

Bw Rajapaksa atajiuzulu tarehe 13 Julai. Waziri Mkuu Wickremesinghe amekubali kujiuzulu.

Spika wa bunge alisema rais aliamua kujiuzulu “ili kuhakikisha makabidhiano ya amani ya mamlaka” na kutoa wito kwa umma “kuheshimu sheria”.

Tangazo hilo lilizua mlipuko wa fataki za sherehe katika jiji hilo.

Viongozi wa kisiasa wanarajiwa kufanya mikutano zaidi kujadili makabidhiano ya madaraka.

Jeshi la Sri Lanka limetoa wito kwa watu kushirikiana na vikosi vya usalama ili kudumisha utulivu.

Baada ya matukio ya Jumamosi, Marekani ilitoa wito kwa uongozi wa Sri Lanka kuchukua hatua haraka kutatua mgogoro wa kiuchumi wa nchi hiyo.

Mmoja wa waandamanaji, Fiona Sirmana, ambaye alikuwa akiandamana kwenye nyumba ya rais, alisema ni wakati wa “kuwaondoa rais na waziri mkuu na kuwa na enzi mpya kwa Sri Lanka”.

“Nina huzuni sana kwamba hawakuenda mapema kwa sababu kama wangeenda mapema kusingekuwa na uharibifu wowote,” aliiambia Reuters.

Makumi ya watu walijeruhiwa katika maandamano ya Jumamosi, na msemaji wa hospitali kuu ya Colombo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu watatu walikuwa wakitibiwa majeraha ya risasi.

Sri Lanka inakabiliwa na mfumuko wa bei na inatatizika kuagiza chakula, mafuta na dawa kutoka nje kutokana na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi nchini humo kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 70.

Imeishiwa na fedha za kigeni na imelazimika kupiga marufuku uuzaji wa petroli na dizeli kwa magari ya kibinafsi, na kusababisha foleni ya siku nyingi kutafuta mafuta.

Matukio ya ajabu ya Jumamosi yalionekana kuwa kilele cha miezi mingi ya maandamano ya amani nchini Sri Lanka.

Umati mkubwa wa watu ulikusanyika kwenye makazi rasmi ya Rais Rajapaksa, wakiimba kauli mbiu na kupeperusha bendera ya taifa kabla ya kuvunja vizuizi na kuingia ndani ya jengo hilo.

Kanda za mtandaoni zilionyesha watu wakirandaranda ndani ya nyumba hiyo na kuogelea katika bwawa la raia, huku wengine wakiokota vitu vya rais na kutumia bafu lake la kifahari.

“Wakati nchi nzima inakabiliwa na matatizo kama haya watu wamekuja hapa kutoa shinikizo hilo. Unapoona jumba hili la kifahari ni dhahiri kwamba hawana muda wa kufanya kazi kwa ajili ya nchi,” Chanuka Jayasuriya aliiambia Reuters.

Bw Rajapaksa aliondoka katika makazo yake rasmi siku ya Ijumaa kama tahadhari ya usalama kabla ya maandamano yaliyopangwa, vyanzo viwili vya wizara ya ulinzi vilisema, kulingana na Reuters.

Ingawa ni makazi rasmi ya Bw Rajapaksa, kwa kawaida analala katika nyumba tofauti iliyo karibu.

Waandamanaji wengi walipiga picha za selfie baada ya kuingia ikulu
Waandamanaji wakishangilia ndani ya makazi ya rais mjini Colombo

Waandamanaji pia walichoma moto nyumba ya kibinafsi ya Waziri Mkuu Wickremesinghe katika mtaa wa matajiri wa Colombo kwa mujibu wa BBC.

Awali alisema alikuwa tayari kujiuzulu ili kuhakikisha usalama wa raia na kutoa nafasi kwa serikali ya vyama vyote, lakini mara baada ya tangazo lake video zilianza kusambaa nyumba yake ikiteketea kwa moto.

Waziri mkuu anaishi na familia yake katika nyumba ya kibinafsi na hutumia makazi yake rasmi kwa shughuli rasmi tu.

Ikiwa kujiuzulu kwa rais na waziri mkuu kunatosha kuwaridhisha waandamanaji bado haijabainika.

“Kujiuzulu pekee hakutakidhi matakwa, lakini angalau huu ni mwanzo kama rais na waziri mkuu wataondoka,” Bhavani Fonseka, mwanasheria maarufu wa haki za binadamu huko Colombo.

“Lazima kuwe na mabadiliko ya amani ya mamlaka ambayo bado hayajaonekana,” alionya.

LEAVE A REPLY