Benjamin Mkapa aliyeiongoza Tanzania kuanzia mwaka 1995-2005 amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliyo jijini Dar es Salaam alipokuwa amepelekwa kwa ajili ya matibabu.
Taarifa ya taifa la Tanzania kuondokewa na rais wake wa awamu ya tatu imetolewa na Rais John Magufuli usiku wa kuamkia leo katika runinga ya taifa TBC.
“Nitamkumbuka kwa mapenzi yake makubwa kwa taifa, ucha Mungu, uchapakazi na utendaji wake katika kujenga uchumi. Hakika Taifa limepoteza nguzo imara. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina”, ameongeza Rais Magufuli katika ukurasa wake wa Twitter.
Nimesikitishwa na kifo cha Mzee wetu Benjamin Mkapa (Rais Mstaafu wa Awamu ya 3). Nitamkumbuka kwa mapenzi yake makubwa kwa Taifa, ucha Mungu, uchapakazi na utendaji wake katika kujenga uchumi. Hakika Taifa limepoteza nguzo imara. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.
— Dr John Magufuli (@MagufuliJP) July 23, 2020
Benjamin Mkapa alizaliwa mwaka 1938. Alipata shahada yake ya kwanza baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda mnamo mwaka 1962 kabla ya kujihakikishia shahada ya uzamili katika nyanja za mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Columbia mwaka 1963.
Kuhusu nyadhifa zake serikalini, Benjamin Mkapa alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada (1982) na hata Marekani (1983-84). Kabla ya hapo aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje (1977-80), na baada ya miaka minne alipata bahati ya kuongoza wizara hiyo kwa muda mwingine wa miaka sita (1984-90).
Mwaka 1995 Benjamin Mkapa alichaguliwa kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipigiwa upatu na mwasisi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Taarifa ya kifo cha Benjamin Mkapa haikueleza alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa gani.
Imeandikwa na Janvier Popote.
[…] Aliaga dunia usiku wa kuamkia jana kwa mujibu wa tangazo la rambirambi lililotolewa na Rais John Mag… […]