Katika ishara ya kuonesha mabadiliko ya kisiasa ya mtu ambaye wakati mmoja alikuwa ametengwa, Rais wa Eritrea Isaias Afwerki amesimama na mshirika wake mkuu, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, kwa kuwapatia wanajeshi wake msaada waliohitaji kupigana na vikosi vya Tigray People’s Liberation Front (TPLF) katika jimbo la Tigray.
Katika hotuba ya hivi karibuni katika bunge la Ethiopia, mshindi huyo wa Tuzo ya Amani Nobel alifichua kwamba Eritrea, iliwapa chakula, mavazi na silaha wanajeshi wa Ethiopia ambao walikuwa wamerudi nyuma wakati TPLF walipowashambulia mara ya kwanza na kuteka kambi zao mjini Tigray, eneo la Ethiopia ambalo linapakana na Eritrea.
Bw. Abiy alisema hatua hiyo iliwawezesha kurudi na kupigana na TPLF, vugu vugu la zamani la wapiganaji karibu 250,000, hadi lilipoondolewa katika utawala wa eneo hilo Novemba 28.
“Watu wa Eritrea wametuonesha… kuwa ni jamaa zetu kwa kusimama nasi wakati mgumu,” aliongeza kusema.
Tamko hilo la Bw Abiy lilikuwa muhimu, japo hakuthibitisha madai kwamba Bw. Isaias, pia alituma wanajeshi wake kusaidia kuwashinda TPLF, adui wa muda mrefu wa kiongozi huyo wa Eritrea ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1993.
Hospitali zadaiwa kushambuliwa
Madai ya kwamba wanajeshi wa Eritrea wameingia Tigray yalitolewa na TPLF, raia waliokuwa wakitoroka mapigano na Waeritrea wanaoishi ndani na nje ya nchi.
“Isaias anatuma Waeritrea wadogo kwenda kufariki Tigray. Vita hivyo pia vitadhoofisha uchumi wetu zaidi. Lakini Isaias atakuwa madarakani kwa muda mrefu. Anawaacha watu katika hali ngumu ili wasipiganie uhuru wao,” alisema Paulos Tesfagiorgis, mwanaharakati wa Eritrea wa kutetea haki ambaye alilazimishwa kukimbilia mafichoni na utawala wa Asmara.
Msemaji wa kitengo cha mambo ya nje ya Marekani pia alisema kulikuwa na “ripoti za kuaminika” za uwepo wa wanajeshi wa Eritrea huko Tigray, na akataja “madai hayo kuwa makubwa”.
Serikali zote mbili zimekanusha ripoti hizo, huku waziri wa mambo ya nje wa Eritrea Osman Saleh Mohammed, akiyataja madai hayo kuwa ”propaganda”
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Gueterres, alisema Bw. Abiy amemhakikishia hakuna wanajeshi wa Eritrea waliongia Tigray, isipokuwa katika maeneo ambayo Ethiopia ilikubali kupeana kufuatia mkataba wa kihistoria wa amani uliofikiwa kati ya nchi hizo mbili mwaka 2018.
Mkataba huo ulimaliza mzozo wa mpakani wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili tangu mwaka 1998-2000, ambao ulisababisha vifo vya watu 100,000.
Kufikiwa kwa mkataba huo kulimfanya Bw. Abiy kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel, ingawa eneo hilo lilikuwa halijahamishiwa Eritrea wakati mzozo wa Tigray ulikuwa umeanza mapema Novemba.
Serikali ya Bw. Abiy imedhibiti kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari, mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kutoa misaada na ya kutetea haki za binadamu kufika Jimbo la Tigray kuchunguza madai ya ukatili uliyofanywa na pande zote katika mzozo huo – ikiwa ni pamoja na hospitali kushambuliwa kutoka ndani ya eneo la Eritrea.
Eritrea haijatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo, yaliyoangaziwa katika taarifa iliyotolewa na mkuu wa UN wa kutetea haki za binadamu. Bw. Abiy amekana akisema wanajeshi wake hawakuua hata raia mmoja katika jimbo la Tigray.
“Vita hivi vimepiganwa gizani. Hakuna mtu anayejua kiwango cha mzozo huo na athari zake,” alisema mchambuzi wa masuala ya Upembe wa Afrika Rashid Abdi mwenye makazi yake Kenya.
Chanzo: BBC