KWA sasa katika gemu la muziki hasa wa Bongo Fleva, kumekuwa na ushindani mkubwa ambao umekuwa ukitia chachu kwenye muziki wa Bongo.
Wasanii wengi wamekuwa wakishindana kwa kuachia kazi kali na kukimbizana kwa spidi kwenye mitandao ya kuuza, kusikiliza, kupakua na kutazama muziki (platforms).
Mabosi wa lebo kubwa Bongo ambazo zinaongoza kwa kufanya poa na hata kunyanyua vipaji mbalimbali hapa nawazungumzia Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au Mondi, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ na Rajabu Abdul ‘Harmonize’ au Harmo.
Lakini katika wote hao, Mondi ameonesha kuwafunika wenzake kwa kuingiza kipao kikubwa kwa mwaka huu japo ni makadirio ya mitandao ambayo inaweka kazi za wasanii na kuuza.
MIKITO NUSUNUSU inakudadavulia kwa kina kazi za wanamuziki hawa kama ifuatavyo:
MONDI
Huyu ni bosi wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), ameongoza kwa kuwafunika wenzake kwenye mitandao ya muziki kwa kukadiriwa kuingiza kiasi cha pesa si chini ya Shilingi Bilioni 3 kwa mwaka.
Mondi anaingiza mapato hayo kwa kupitia ngoma zake ambazo zinasifika kukimbiza mitandaoni huko. Ngoma kali ambazo zimekimbiza sana kwenye mtandao wa YouTube ni pamoja na Jeje yenye watazamaji milioni 35, Hainisumbui yenye watazamaji milioni 1.5, Gere yenye watazamaji milioni 20 mpaka sasa, Ongeza (milioni 1.3), zote zikitazamwa kwa jumla ya milioni 57, kwenye mtandao wa YouTube tu na bado kuendelea kukimbiza mitandao mingine ya kusikiliza na kuuza muziki.
Mbali na ngoma hizo pia album yake ya A Boy From Tandale, imechangia kuongeza mapato yake na kufikia kiwango hicho.
KIBA
Ali Saleh Kiba almaarufu King Kiba, huyu ni bosi wa Lebo ya King’s Music ambayo nayo inasimama katika lebo bora hapa Bongo.
Kiba ni mkongwe kwenye gemu hili la muziki na anasifika kutoa kazi kali japo sio kwa mpigo kama ilivyo kwa wasanii wengine.
Kiba anakadiriwa kuingiza mapato si chini ya Shilingi Milioni 139 kwa mwaka kutokana na ngoma zake kutazamwa na kusikilizwa sana mitandaoni.
Ngoma zake zilizofanya poa kwa kutazamwa sana kwenye mtandao wa YouTube kwa mwaka huu ni pamoja na Dodo yenye watazamaji milioni 10, So Hot yenye watazamaji milioni 3.2, Mediocre (milioni 3) na Mshumaa (milioni 6). Mpaka sasa zote kwa jumla zikitazamwa na mara milioni 22 kwenye mtandao wa YouTube na kukimbiza pia kwenye mitandao mingine ya muziki.
HARMONIZE
C.E.O wa Lebo ya Konde Music Gang, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ au Harmo, ni mwanamuziki ambaye anasifika kwa kutoa kazi kali tangu akiwa na lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) ambapo alijitoa na kuanzisha lebo yake mwenyewe.
Harmo anakadiriwa kuingiza mapato si chini ya Bilioni 1 kwa mwaka kutokana na kazi zake kukimbiza kwenye mitandao ya kusikiliza, kupakua, kuuza na kutazama muziki (platforms).
Ngoma zake zilizoongoza kwa kutazamwa sana kwenye mtandao wa YouTube kwa mwaka huu ni pamoja na, Jeshi yenye watazamaji milioni 4, Fall in Love yenye watazamaji milioni 4, Mpaka Kesho (milioni 3), Wife (milioni 3), Mama (milioni 2), zote zikitazamwa mara milioni 16 mpaka sasa kwenye mtandao wa YouTube.
Album yake ya Afro East aliyoizindua mwaka huu ikiwa imebeba ngoma 18 nayo imetajwa kuingiza mauzo mazuri mitandaoni.
Chanzo: Global Publishers