WAKATI tukielekea ukingoni kabisa mwa mwaka 2020, wapo wasanii wengi wamefanya vizuri kwa mwaka huu ambapo nyimbo zao zimesikilizwa zaidi kwenye mitandao mbalimbali lakini pia zimechezwa kwenye kumbi mbalimbali za starehe.
RISASI JUMAMOSI limechimba kwa upande wa wasanii wa kike na kukuletea orodha ya wasanii wanne ambao wametikisa zaidi kwa nyimbo zao licha ya mwaka huu kukumbwa na janga la ugonjwa wa Corona:
NANDY
Faustina Charles Mfinanga ndilo jina lake halisi. Wengi wanamfahamu zaidi kwa jina la Nandy, huyu amefanya vizuri mwaka huu ambapo amefanikiwa kuachia nyimbo mbalimbali ambazo kimsingi zimemweka juu.
Miongoni mwa nyimbo zake zilizofanya vizuri ni pamoja na Acha Lizame aliomshirikisha Rajabu Abdul ‘Harmonize’ yenye watazamaji 2, 234, 168 YouTube, Na Nusu (2, 234, 168), Nibakishie aliyomshirikisha Ali Saleh Kiba ‘AliKiba’ (3, 071, 262) na Do Me aliyomshirikisha Billnass iliyotazamwa na watu 2, 188, 254.
ZUCHU
Zuhura Othman ‘Zuchu’ ni msanii ambaye kimsingi ameiandika historia ya kutoka mwaka huu na kufanikiwa kutikisa kwenye ulimwengu wa Bongo Fleva. Nyimbo zake ziliweza kutoboa kwenye kipindi kigumu cha ugonjwa wa Corona, zikafanya vizuri sana.
Miongoni mwa nyimbo zake zilizofanya vizuri mwaka huu ni pamoja na Wana yenye watazamaji Mil. 9.6, Litawachoma aliyomshirikisha Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ (Mil. 10), Cheche featuring Mondi (Mil. 13) na Nisamehe ambao umetazamwa na watu Mil. 7.9.
MAUA SAMA
Maua Sama amekuwa na muendelezo mzuri wa kuachia ngoma zake. Mwaka huu hakuwa nyuma kwani ameachia kazi zake kali ambazo zimemfanya aendelee kupigwa kwenye kumbi mbalimbali za starehe na kwenye vituo vya redio na televisheni.
Nyimbo ambazo zimembeba mwaka huu ni pamoja na Nioneshe iliyotazamwa YouTube na watu 850, 000 na Kan Dance ambayo ina wafuasi 848,000. Ukirudi nyuma kidogo, Maua Sama anayo rekodi nzuri, wimbo wake wa Iokote alioutoa miaka miwili iliyopita, una jumla ya wafuasi Mil. 20 mpaka sasa.
LADY JAYDEE
Hakuna ubishi Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ ndiye msanii mkongwe zaidi kwenye wasanii wengi wa kike Bongo. Kwa upande wake wake ameendelea kukimbiza mwaka huu kwa kuachia nyimbo nzuri lakini pia kufanya matamasha makubwa ambayo yamedhihirisha kwamba anakubalika kwa kukusanya ‘kijiji’ chake.
Shoo yake ya miaka 20 aliyoifanya hivi karibuni ilidhihirisha hilo. Watu walikuwa wengi lakini pia hivi karibuni aliachia mkwaju wake unaokwenda kwa jina la Ni Hapo ambayo amemshirikisha mwamba kutoka Kaskazini, John Saimon ‘Joh Makini’ ambao unafanya vizuri.