Rostam Aziz

Mfanyabiashara Rostam Aziz amesema uwekezaji nchini Tanzania na Kenya haufanani akibainisha kuwa ni rahisi kuwekeza katika nchi moja na ngumu kwa nchi nyingine na kutaka suala hilo kufanyiwa kazi ili kutogharimu uhusiano wa nchi hizo mbili.

Rostam ametoa kauli hiyo Jumatano Mei 5, 2021  katika kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika nchini Kenya na kuhudhuriwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta.

“Ni rahisi sana kwa Kenya kuja Tanzania kuwekeza lakini hali ni tofauti kwa upande wa pili na mifano ni mingi sana. Kuna kampuni 530 za Kenya ambazo zimewekeza zaidi ya Dola 1.7 bilioni za Marekani nchini Tanzania lakini kuna kampuni 30 tu za Tanzania zilizofanikiwa kuwekeza nchini Kenya kwa uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 50 pekee.”

“Uhusiano huu si ule wa kujenga uchumi kati ya mataifa haya mawili na iwapo tutashindwa kuufanyia kazi basi hatutaweza kufanikiwa kutimiza malengo yetu,” amesema Rostam.

Amesema mwaka 2017 alikwenda Kenya na kufanya mazungumzo na Kenyatta aliyemtaka awekeze nchini humo lakini hadi sasa suala hilo halijafanyiwa kazi.

“Rais Kenyatta aliniomba niwekeze nchini Kenya na aliniuliza kwamba ningependa kuwekeza kwenye nini,  nikamwambia naona kuna fursa kwa upande wa gesi, sasa imepita miaka mitatu bado sijapata majibu kuhusu uwekezaji niliotaka kufanya ambao ungegharimu Dola za Marekani milioni 130.”

“Iwapo hatutatengeneza mahusiano mazuri ya uwekezaji kati ya Tanzania na Kenya basi mahusiano yaliyopo hayataweza kudumu, ningependa kusisitiza kwamba kunahitajika usawa kwa pande zote mbili ili tuweze kukuza uchumi kati ya mataifa haya mawili,” amesema Rostam.

Chanzo: Mwananchi

LEAVE A REPLY